NENO LA LEO | Mithali 3:5-6 Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe…

Mithali 3:5-6

5. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; 6. Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.

TAFAKARI

Kuna faida kubwa katika kuishi maisha ya kumtegemea Mungu. Mzaburi Daudi anasema, “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula. Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa.”(Zaburi 37:25-26).
Mfalme Sulemani alijifunza hili kwa Baba yake Daudi ndo maana akasema unampomtumania Bwana kwa moyo wako wote, usipotegemea akili zako. Katika njia unazopotia mkiri yeye, basi Mungu atanyosha mapito yako. Kwa lugha nyingine, hatakuacha, hataacha watoto wako wawe omba omba, bali atakupa kukopesha mataifa mengi na kukubariki uingiapo na utokapo, mjini na kijijini, ujanani na uzeeni na kubariki kizazi chako.

SALA

Bwana Mungu, nipe kukuamini Katika kila eneo la maisha yangu. Nisadie nifungue moyo wangu na ondoa kila hali ya kutoamini ndani mwangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Luka 17:6 Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii…

Luka 17:6

Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.

TAFAKARI

Kuna mambo tunakutana nayo kila siku katika maisha ambayo yanatakiwa tuwe na imani. Yesu anatufunisha kuwa tukiwa na imani kiasi cha chembe ya haradali tunaweza kuwambia mti ung’oke na ukapandwe baharini, nao utatutii. Inawezekana kuna tatizo katika maisha yako ambalo linakua kizuizi cha mipango yako. Siku ya leo nataka nikukumbushe kuwa tumia imani kama silaha ya kukusadia kulishinda hilo tatizo lako. Amini kuwa Mungu ana uwezo wa kukushindia lolote unalopitia. Amini kuwa atakuwa pamoja nawe katika njia yeyote unayopitia na mwisho wa siku utakuwa mshindi.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kusimama katika imani na kutumia imani yangu kushinda majaribu yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | MITHALI 14:10 Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake…

MITHALI 14:10

Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake.

TAFAKARI

Mara nyingi tumejikuta tunawafariji wenzetu wanakuwa wanapitia magumu katika maisha. Ni rahisi kuona kwa njee mtu anavyoonekana ameumia lakini wakati mwengine tunashindwa kuelewa kiwango cha masumbufu ya huyo mtu ndani mwake. Maandiko yanasema moyo huujua uchungu wa nafsi yake, kwa lugha nyingine uchungu wa jambo hujulikana na yule mtu anayepitia. Kisha inaendelea wala mgeni haishiriki furaha yake, hii inaonyesha pia ni ngumu kujua namna gani mtu anaweza furahi jambo fulani katika maisha yake. Kwa kufahamu yote haya imetupasa kuwa na huruma na kujifunza kuchukuliana na watu. Kuna wengi wapo jinsi walivyo kwa sababu wana machungu mengi ndani, wengine wana historia zenye uchungu mwingi. Unaweza mwona anapendeza kwa njee na mara nyingine anaonekana amefanikiwa lakini si rahisi kuona vidonda vyake ndani. Tuombeane na kuchukuliana katika safari hii ya maisha hapa duniani.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kuchukuliana na watu wote wananizunguka nipe kuwaombea zaidi kuliko kuwalaumu kwenye mapungufu yao nikijua kuwa nakutumikia Mungu mwenye huruma unihurumiaye kila itwapo leo. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | ZABURI 71: 1 – 3 Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe…

ZABURI 71: 1 – 3

Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe.
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.

TAFAKARI

Biblia inazungumzia kuhusu aibu ya milele(Daniel 12:2), hii ni aibu ambayo watapata watu waliishi maisha ya uovu kwenye dunia hii baada ya hukumu ya Mungu. Mara nyingi tunapoongea kuhusu mauti, hukumu na mauti ya pili kuna watu wanasikiliza kama stori tu za kutisha lakini ukweli hawatulii maanani. Mfalme Daudi aliamua kumkimbilia Bwana ili asije kuishia kuaibika milele. Alishajua kuwa kuwa kuna aibu waovu wataipata wasipotubu katika maisha haya. Kuna vifungu vingi kwenye maandiko vinavyoonyesha hili lakini kitu kimoja cha kujifunza ni kwamba ipo siku wote tutahukumiwa. Ipo siku wote tutasimama mbele za Mungu na kutoa hesabu ya makosa yetu. Tusije kuja kusahau hili, Mungu atusadie tuishi maisha ya hofu yake na kiasi ili ikifika wakati tupate kuhesabiwa haki pamoja na wale wote walio subiri ujio wa Mwana wa pendo lake ambaye ni Yesu.

SALA

Mungu wangu naomba nisadie niishi maisha ya toba. Nadondoka katika mambo mengi na nakosea kwenye mengi. Nipe kutubu kwa pale napokosea ili niweze tembea kwenye neema yako. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Wagalatia 2:9 Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara…

Wagalatia 2:9

Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara.

TAFAKARI

Yakobo, Kefa ambaye ni Petro na Yohana walikuwa ni mitume walikuwa pamoja na Yesu. Walipoona neema ilikuwa katika maisha ya Paulo na Barnaba waliwapa mkono wa kuume washirika kama ishara kuwa wametambua huduma yao na wakawaruhusu kwenda kuuhubiri Injili kwa mataifa. Tuna vurugu nyingi sana katika kanisa la leo kwa sababu kuna watu walimpokea Roho Mtakatifu na wakajua mistari miwili mitatu na hujiona kuwa wanafaa kuwa watumishi na kutafuta nafasi za kutumika hata kama kwa lazima. Ni mapenzi ya Mungu wote tuokolewe na tuufikie ule uzima, lakini sio kusudi lake wote tuwe waalimu wa Neno lake kama Yakobo 3:1 inavyosema, “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.” Kama kuna mambo au jambo bado hujapata neema ya kulielewa basi ni hekima ukanyamaza kuliko kutoka na kufundisha tofauti na kuishia kupotosha kanisa. Mungu atusadie tuweze kuwa wapole na wenyenyekevu katika mambo yote yanayohusu kumtumikia.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze simama kwenye wito wangu. Nisije lazimisha kufanya kitu ambacho Mungu hukukusudia nifanye kwenye kanisa lako. Bali nipe neema ya kujua na kutembea kwenye kusudi lako. Kwa Jina Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org