NENO LA LEO | Marko 12: 43 Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninawaambia hakika, huyu mjane ametoa zaidi kuliko wote…

Marko 12: 43

Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninawaambia hakika, huyu mjane ametoa zaidi kuliko wote!

TAFAKARI

SADAKA! Mara NYINGI tunaangalia WINGI wa sadaka zetu na tunasahau HALI ya MIOYO yetu. Kama WATOAJI wa SADAKA, thamani halisi ya sadaka zetu ipo ndani ya mioyo yetu. Kisa cha mwanamke, tena mjane kinatupa nafasi ya kujifunza kuhusu THAMANI ya SADAKA zetu. Kwa mujibu wa mazungumzo ya YESU na WANAFUNZI wake, thamani ya sadaka haimo ndani ya UKUBWA au UDOGO wa sadaka zetu. Thamani halisi ya SADAKA inategemea MOYO uliotoa na wala sio KIWANGO cha fedha tuliyoitoa. Yesu aliposimama karibu na sanduku la HAZINA, aliwaona watu wakitoa sadaka zao. Matajiri walitoa fedha NYINGI. Mama mjane alitoa “nusu pesa.” Yesu anaangalia moyo wa MTU. Ndiyo maana akasema, “huyu mjane ametoa zaidi kuliko hawa wote.” Ametoa kile alichonacho, na WENGINE walitoa katika ZIADA. Neno “ziada” ni kile kinachobakia. Mungu atusaidie kuitambua SIRI, hii. Siri hii itatusaidia kuongeza THAMANI ya SADAKA zetu mbele ya Mungu wetu, Amina.

SALA

Ee Mungu, tunakuomba utusaidie tuwe na uwezo wa kutanguliza mioyo yetu madhabahuni pako na wala siyo sadaka zetu. Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Luka Mtakatifu 17:21 ….tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu…

Luka Mtakatifu 17:21

….tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.

TAFAKARI

“Mungu anaishi wapi?” Swali aliuliza mtoto mmoja wa miaka 4. Mzee mmoja mwenye hekima, akamchukuwa na kumwongoza mpaka kisimani. Mzee akajibu, akamwambia yule mtoto, “ angalia ndani ya haya maji. Je! Unaona nini?” Mtoto akajibu, “naiona sura yangu.” Yule mzee akamwambia, “hapo ndipo mahali Mungu anapoishi. Mungu anaishi ndani yeko.” Jibu hili linafanana kabisa na jibu la Bwana Yesu, “ufalme wa Mungu umo ndani yenu.” Wakristo wengi wa leo tumeendelea kuuliza swali hili. Somo la leo linatukumbusha kuwa ufalme wa Mungu siyo eneo fulani la kijiografia. Ufalme wa Mungu ni MAMLAKA na UWEZA wa Mungu ambavyo vimo ndani ya wana wa Mungu, kama tusomavyo “..mtu akisikia sauti yangu, na kufungua mlango, nitaingia kwake,.” (Ufunuo 3:20).

SALA

Baba yetu wa mbinguni, tunakuomba utupe uwezo wa kukukaribisha maishani mwetu daima milele na milele , Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Zaburi 121:1-2 Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi…

Zaburi 121:1-2

Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.

TAFAKARI

Mungu ndiye aliye muumba mwanadamu, alituumba mimi na wewe kwa sura na mfano wake. Akatupa dunia ili tupate kuitawala na kuimiliki. Tulipoanguka katika dhambi alimtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo ili aje kutukomboa na kuturudisha kwenye nafasi ambayo shetani alichukua. Huyu Mungu ndiye msaada wetu, yeye pekee ndiye kimbilio letu na faraja yetu. Inawezekana ndugu unapitia katika majaribu, inawezekana umeamka asubuhi ya leo ukiwa na mawazo mengi sana ulitamani usiku uwe mrefu zaidi. Nataka nikutie moyo kuwa yupo Mungu. Yupo alikuweka hapa duniani, hajakuweka kwa bahati mbaya na yupo tayari kukusadia kwenye shida yako. Nenda mkimbilie yeye siku ya leo.

SALA

Mungu Baba, uliye mbinguni Jina lako litukuzwe siku ya leo. Naleta shida zangu mbele zako. Unajua yote nayopitia, naomba unitende muujiza siku ya leo nipate kuona mkono wako maishani mwangu. kwa Jina la Yesu nimeomba, Amina.©

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Warumi 3:23 Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu…

Warumi 3:23

Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.

TAFAKARI

Wote sisi tumetenda dhambi katika wakati mmoja au mwingine. Hakuna hata mmoja wetu anayeweza simama kwa ujasiri na kusema yeye hajawahi kutenda dhambi. Hakuna hata mmoja wetu ambaye amepona.
Hakuna mwanadamu anayeweza kujikomboa kwa nguvu zake mwenyewe, wote tumepungukiwa na utukufu wa Mungu. Wote tunahitaji mkombozi.Wote tunahitaji msamaha wa dhambi. Kwa hiyo usiwe mwepesi wa kunyosha kidole au kujiona wewe ni bora kuliko wengine bali kaa chini na uombe Mungu akurehemu. Omba kwamba Mungu akusadie uishi maisha ya kumpendeza.
Salimisha maisha yako kwake ili siku moja upate kurithi uzima wa milele.

SALA

Mungu wangu, nimetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wako. Naomba unisamehe na kunirehemu. Mara nyingine tena nasalimisha maisha yangu yote kwako. Nisadie niweze shinda dhambi na kila aina ya vishawishi toka kwa yule adui. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org