NENO LA LEO: Marko 10:21-22 Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia,. . .

NENO LA LEO: Marko 10:21-22 Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

TAFAKARI: Mara nyingi mali na anasa za dunia hii huwa zinatuzuia kumfuata Yesu. Kuna kijana kwenye maandiko alikuwa na mali nyingi, na alipouliza afanye nini ili arithi Ufalme wa Mbinguni, alijibiwa kuwa akauze vyote alivyo navyo kisha amfuate Yesu. Huyu kijana alihuzunika maana alikuwa na mali nyingi. Kuna mambo tunayafanya katika maisha haya ambayo tukiendelea kufanya yanaweza kutuzuia kurithi ule ufalme ujao. Sijui ni jambo gani ndugu yangu hutaki kuliachia ili upate kutana na Yesu maishani mwako. Sijui ni mtu gani au kitu gani kinazuia usimfahamu mwana wa Mungu kiundani zaidi. Leo nataka nikutie moyo kuwa neema bado ipo, ukikubali na kutii sauti ya Bwana Yesu; atakusamehe na kukuokoa toka kwenye dhambi na mauti.

SALA: Mungu wangu, nisadie niweze kusikia sauti ya wito wako na kukubali kukufuata. Kwa Jina la Yesu, Amina.
(C)IYK-NENO
www.iykcolumbus.org