NENO LA LEO | 2 Wakorintho 12:9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu…

2 Wakorintho 12:9

Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

TAFAKARI

Ndani ya Yesu kuna neema ya Mungu inayotufunika katika madhaifu yetu. Kuna neema inayotulinda ili tusivuke mipaka na kufanya mambo ya aibu katika maisha. Bila hiyo neema kila mmoja wetu anaweza kufanya lolote lile ambalo watu wengine wasio na Mungu hufanya. Kama una udhaifu ambao unakusumbua kaitka maisha yako, nenda mbele za Mungu na uombe neema yake ikusadie kushinda huo udhaifu. Omba neema yake ipate kukufunika ili adui asije akautumia udhaifu wako kwa ajili ya makusudi yake. Unapokiri udhaifu wako mbele za Mungu na kujisalimisha mikononi mwake. Atakupatia nguvu ya kushinda, kusonga mbele na kufanikiwa katika njia yako.

SALA

Mungu wangu, nakabidhi udhaifu wangu mikononi mwako. Naomba unisafishe na kunisaidia niweze kuishinda. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Waefeso 3:17-19 Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo…

Waefeso 3:17-19

Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.

TAFAKARI

Upendo katika kanisa la Mungu umepoa. Wengi tunajipenda wenyewe kuliko tunavyopenda wengine. Kuna kipindi watu walikuwa wako tayari kuomba na kufunga kwa ajili ya wengine. Watu walikuwa wapo tayari kutumia mali zao na muda wao kusadia wengine. Tumefika kipindi ambapo watu ni wabinafsi na wanatanguliza mambo yao na kushindwa kuwatanguliza wengine. Tunapoamua kupenda wengine, Mungu hutupa neema ya kutusadia kuwapenda hao watu. Najua kuwa kuna watu ambao kwa namna za kibinadamu wanastahili kutoonyeshwa upendo lakini Neno la Mungu linatufundisha kuwapenda hata kama hao watu ni maadui zetu. Siku ya leo mwombe Mungu akupe nguvu za kupenda watu; mwombe akupe nguvu kusamehe wale walikuumiza. Upendo utakundisha kuachilia na kuwachukulia watu katika madhaifu yao. Upendo utakuwezesha kuwatumikia wengine kwenye mwili wa Kristo kama vile ambavyo Mungu angetaka iwe.

SALA

Mungu wangu, naomba unipe nguvu niweze kupenda jirani zangu. Nipe nguvu ya kusamehe, kusahau na kuachilia. Nisadie niwapende hata maadui zangu, na kuendelea kuwaombea. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 2 Wathesalonike 3:3 Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu…

2 Wathesalonike 3:3

Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.

TAFAKARI

Sifa moja ya Mungu ambaye tunamtumikia ndani ya Kristo Yesu, ni kwamba ni Mungu mwaminifu. Ni Mungu ambaye hutimiza ahadi zake kwa wanadamu na kuwatunza wale wote wampendao. Tunajua kuwa kuna nguvu mbili zishindanazo katika ulimwengu huu, nguvu za giza (za shetani) na nguvu za nuru, za Bwana wetu Yesu Kristo. Sisi tulio ndani ya Kristo tunajua kuwa nguvu za giza zinaweza kupambana dhidi yetu lakini hazitaweza kutushinda maana aliye ndani mwetu ni mkuu kuliko aliye ulimwenguni. Nataka nikutie moyo kuwa usimwogope shetani wala wakala wake yeyote. Mungu hatamruhusu akuonee wala kukudhuru. Atakulinda wewe na familia yako, na hata utakapopita kwenye bonde la uvuli wa mauti,yeye atakulinda na atakuepusha na mabaya yote na kukufanya imara ndani ya Kristo Yesu.

SALA

Mungu wangu na Baba yangu, tazama maisha yangu yapo mikononi mwako. Ninazidi kujikabidhi kwako siku ya leo, naomba uzidi kunifunika kwa damu ya mwanao Yesu Kristo. Unitunze kwenye pendo lako ili niweze kutembea kwenye amani yako. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Zaburi 138:1 Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi…

Zaburi 138:1

Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

TAFAKARI

Mungu wetu anapendezwa na moyo wenye shukrani. Tunapokuwa tunapitia vipindi mbali mbali kwenye maisha inatupasa kujifunza kumshukuru Mungu katika kila jambo. Ni rahisi kumshukuru Mungu pale tunapo pandishwa cheo, ndoa zetu zinapokuwa na amani, tunapokuwa kwenye afya njema na tunapopata mafanikio kwenye shughuli zetu za kila siku. Inakuwa ngumu kumshukuru Mungu pale mambo yanapoenda kinyume na matarajio yetu. Tunapojifunza kumshukuru Mungu hata nyakati za shida, Mungu huliona hilo na hushuka chini ili apate kutuokoa. Nataka nikutie moyo ndugu yangu. Mshukuru Mungu ukiwa kwenye bonde na ukiwa kwenye kilele ,na tambua katika yote unayopitia yeye yupo pamoja nawe ili kukusaidia.

SALA

Bwana Mungu, asante kwa kila jambo katika maisha yangu. Pokea sifa kwa yote unayo nitendea, Jina lako lipate kuinuliwa milele. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org