NENO LA LEO | Zaburi 125:1 Wamtumainio BWANA ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele…

Zaburi 125:1

Wamtumainio BWANA ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele.

TAFAKARI

Sisi tulio ndani ya Kristo ambao tumeamua kumfuata yeye na kuacha njia zetu mbaya tunajua umuhimu wa kumtumainia Mungu kwenye maisha yetu ya kila siku. Watu wa ulimwengu huu hutegemea akili zako matokeo yake mwisho wa siku hugonga mwamba na kukosa tumaini. Tuna watu ambao wanasumbuliwa na roho chafu mfano kama mapepo. Hizi roho zinawanyima raha, zinawaletea ndoto mbali mbali chafu na wakati mwengine za kutisha. Huwa zinachangia kwenye kuharibu mahusiano yao na watu wengine na mara nyingine huleta magonjwa na madhaifu katika miili. Kwa akili na utaalamu wa kibinadamu hutuwezi kutoa pepo ndani ya mtu. Waganga pia hawawezi maana wana tumikia kusudi hilo hilo la ufalme wa giza. Dawa pekee ni Yesu. Ukimwamini na kumtumaini basi yeye atakufungua toka katika vifungo vyote vya giza, atakuponya magonjwa yako na kukusamehe dhambi zako. Weka tumaini lako kwake siku ya leo, na hutakuja kujutia uamuzi wako kamwe.

SALA

Bwana Mungu, naomba kupitia nguvu ya Roho wako Mtakatifu unifungue na kila aina ya vifungo vya mapepo, majini na mizimu ya ukoo. Niweke huru na kila aina ya laana, mikosi na hali ya kutofanikiwa kwa Jina la Yesu. Nisadie niweze tembea katika kusudi lako siku zote za maisha yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Wafilipi 4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu…

Wafilipi 4:13

Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

TAFAKARI

Kuna wakati kwenye maisha sote huwa tunachoka. Inawezekana umechoshwa na ndoa yako, umejikuta unapitia jaribu katika kila kona ya ndoa yako kuanzia kwa wakwe mpaka kwenye amani yenu humo ndani. Pia inawezekana umechoshwa na maisha ya nchi hii, kila unalojaribu halifanikiwi. Vibali huna na imefika wakati umekata tamaa kabisa unaishi maana kuna watu wanakutegemea kwa hiyo huna jinsi. Pia inawezekana umechoshwa na hali ya kuwa kapela, umemwomba Mungu upate mwenzi wa maisha, umejaribu kuingia kwenye mahusiano ya hapa na pale lakini yote mwisho ya siku yameishia kwenye maumivu. Siku ya leo nina habari njema kwa ajili yako. Kuwa yupo Mungu atiaye nguvu, Mungu aliyekuleta kwenye nchi hii yupo! Mungu aliyekupa hiyo ndoa yako yupo! Mungu aliyekuumba wewe alisha kuandalia mwenzi wako wa maisha. Nataka nikutie moyo jitie nguvu katika Bwana asubuhi ya leo, mwamini yeye maana yupo mbioni kukujibu maombi yako.

SALA

Mungu wangu na Baba yangu, kuna mambo mengi yamenichosha kwa kweli. Nina majuto mengi na sina hata mwelekeo wa kesho yangu. Naomba unitie nguvu siku ya leo, nisadie niweze kusimama kwa imani nikijua kuwa hata sasa umeshanisadia. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Yohana 14:16-17 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye Roho wa kweli…

Yohana 14:16-17

Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui, bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu.

TAFAKARI

Watu wengi huwa wanasahau nafasi ya Roho Mtakatifu katika kanisa na maisha ya kila mmoja wetu. Bwana Yesu alivyoenda kwa Baba alituachia Roho wa Mungu awe msadizi wetu katika yote tunayopitia katika maisha haya. Mungu hakukusudia tuhangaike peke yetu kama yatima. Alituachia Roho wake ili apate kutushauri na kutufunulia mambo ambayo yapo mbele yetu. Wakristo wengi hawajui kazi ya Roho wa Mungu kwenye maisha yao ndo maana wengi wanaishi bila tumaini. Yeye ndiye mfariji wetu na tumaini letu wakati wa shida. Yeye ndiye atupaye hekima ya kupambana na shida za maisha haya. Tukimtegemea atatupa nguvu za kushinda dhambi na kushinda majaribu. Siku ya leo mwombe Mungu akufunulie Roho wake kwenye maisha yako. Mwombe akujaze kwa upya na nguvu za Roho wake Mtakatifu. Omba akupe kutembea kwenye imani iliyo ndani ya Yesu Kristo Bwana wetu siku zote za maisha yako.

SALA

Mungu Baba, naomba umtume Roho wako kwenye maisha yangu. Natamani nijazwe kwa upya na nguvu ya Roho wako siku ya leo. Natamani nimwone akinigusa na kubadilisha maisha yangu. Natamani kuona akichukua hofu zangu na huzuni zangu. Karibu Roho Mtakatifu kwenye maisha yangu ili upate kutimiza mapenzi yako yote. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 2 Wakorintho 12:9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu…

2 Wakorintho 12:9

Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

TAFAKARI

Ndani ya Yesu kuna neema ya Mungu inayotufunika katika madhaifu yetu. Kuna neema inayotulinda ili tusivuke mipaka na kufanya mambo ya aibu katika maisha. Bila hiyo neema kila mmoja wetu anaweza kufanya lolote lile ambalo watu wengine wasio na Mungu hufanya. Kama una udhaifu ambao unakusumbua kaitka maisha yako, nenda mbele za Mungu na uombe neema yake ikusadie kushinda huo udhaifu. Omba neema yake ipate kukufunika ili adui asije akautumia udhaifu wako kwa ajili ya makusudi yake. Unapokiri udhaifu wako mbele za Mungu na kujisalimisha mikononi mwake. Atakupatia nguvu ya kushinda, kusonga mbele na kufanikiwa katika njia yako.

SALA

Mungu wangu, nakabidhi udhaifu wangu mikononi mwako. Naomba unisafishe na kunisaidia niweze kuishinda. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org