NENO LA LEO | Yohana 16:13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote…

Yohana 16:13

Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

TAFAKARI

Katika kanisa tunajitahidi kuhubiri mambo yote, tunamhubiri Yesu na wokovu wake. Tunafundisha watu waache dhambi na waache matendo maovu na kutenda mema. Yote haya ni mambo mema na mazuri lakini wengi wetu tumeisahau nafasi ya Roho Mtakatifu katika mwili wa Kristo. Naamini kwa wengi habari za Roho Mtakatifu ni ngeni au wengine wanahisi labda hakuna haja sana ya kumfahamu. Kwa nilichojifunza mimi, ukitaka kuelewa kazi ya Roho Mtakatifu katika mwili wa Kristo ni sawa na engine kwenye gari. Pasipo yeye hakuna linaweza kufanyika na likafanikiwa hata kama haonekani. Kuna haja ya kumrudisha Roho Mtakatifu kanisani, kuna haja ya kuanza kujifunza maandiko yanasema nini juu ya Roho wa Bwana. Ni maombi yangu, Mungu atafungua namna ya sisi tupate kumfahamu zaidi huyu msadizi aliyemtuma kwetu apate kukaa na sisi hata milele.

SALA

Bwana Mungu, naomba nisadie niweze kumfahamu Roho wako Mtakatifu. Nisadie niweze pata mafundisho ili nipate kufahamu na kuelewa kazi yake katika mwili wa Kristo na ndani ya maisha yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Matendo 4:12. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo…

Matendo 4:12.

Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.

TAFAKARI

Jina la Yesu lina nguvu. Lina nguvu ya kuokoa, kuponya, kufungua na kusamehe ndambi. “Jina la Yesu ni jina lipitalo kila jina; kwa jina la Yesu kila goti linapigwa, na vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi utakiri kuwa YESU KRISTO ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba, Wafilipi 2:10-11.” Hili ndo jina tuliyopewa sisi tulio ndani ya Kristo Yesu, ndo jina lenye nguvu ya kutuokoa kama Nabii Yoeli alivyotabiri kuwa itafika wakati ambao, “mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa, Yoeli 2:32”. Nataka kukutia moyo siku ya leo liite jina la Bwana, na wewe utapokea uponyaji wako.

SALA

Mungu Baba, asante kwa zawadi ya Jina la Yesu. Yesu wangu nakukaribisha maishani mwangu, fanyika kuwa Bwana na mwokozi, ukafanyike kuwa Mfalme na mtawala wa maisha yangu. Nasalimisha kila sehemu ya maisha yangu, Bwana Yesu uwe kiongozi wangu tangu sasa na hata milele. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 1 Wakorintho 10:13 Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu, ila Mungu ni mwaminifu, ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo…

1 Wakorintho 10:13

Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili muweze kustahimili.

TAFAKARI

Kila mmoja kwa namna moja au nyingine amewahi kujaribiwa. Inawezekana kuna wengine tunapita kwenye majaribu wakati huu; au unaishi na mtu au rafiki ambaye kila itwapo leo anakujaribu. Kwa jambo lolote unalopitia au utakalopitia hapo mbeleni, ujue kuna mlango wa kutokea Mungu ameshakuandalia. Mungu hataruhusu ujaribiwe kupita uwezavyo, chochote unachopitia sasa hivi ujue Mungu alishaona una uwezo wa kustahimili ndo maana akakiruhusu. Siku ya leo nataka ujipe moyo na ujue ndani yako kuna nguvu tayari ya kushinda hilo jaribu. Mungu atakuponya na kukutoa katika hilo jaribu ukiendelea kusimama katika imani ndani yake.

SALA

Mungu wangu, nakushukuru kwa zawadi ya maisha. Naomba nisadie nishinde majaribu yote nayopitia katika maisha haya. Nisadie niweze kujifunza katika kila nalopitia ili nifanyike kuwa faraja kwa wengine watakapitia pale nilipopitia. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Wafilipi 3:12-14 Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika…

Wafilipi 3:12-14

Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.

TAFAKARI

Najua wengi wetu mara nyingi tunadondoka kisha tunasimama tena. Kuna wakati mwengine kwa ajili ya kudondoka kwetu mara kwa mara tunakata tamaa kuwa ipo siku na sisi tutakuja kusimama vizuri na Mungu. Tunatamani kusimama kama wengine tunavyowaona wamesimama vizuri na Mungu. Siku ya leo nataka nikutie moyo kuwa hakuna aliyefika bali wote tunakaza mwendo ili tupate kulishika lile ambalo Bwana wetu Yesu Kristo ameweka mbele yetu. Kinachotakiwa nikusahau yaliyo nyuma, tukiyachumilia yaliyo mbele, tukaze mwendo, ili tufikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Usikate tamaa endelea kumsogelea Mungu kila Siku.

SALA

Mungu wangu, nakushukuru kwa kunipenda. Naomba unitie nguvu niweze kusimama tena kila saa nitakayo jikuta naanguka. Naomba haya katika Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org