NENO LA LEO | Mithali 23 : 22-25 Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee…

Mithali 23 : 22-25

Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee. Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu. Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia. Na wafurahi baba yako na mama yako; Na afurahi aliyekuzaa.

TAFAKARI

Wazazi wetu ndio wawakilishi wa Mungu katika maisha yetu duniani hapa. Mtu anayewazarau wazazi wake hawezi kupata thawabu mbele ya mwenyezi Mungu. Huwezi kujidai kuwa unampenda Mungu huku unawazarau wazazi wako. Neno linatuagiza kuwasikiliza na kuwapenda wazazi wetu muda wao wote hapa duniani.Furaha ya wazazi wetu ndio mafanikio yetu!

SALA

Tunakushukuru Mungu wetu kwa Baraka ya wazazi uliotupa. Tunakuomba utusamehe pale tunapotetereka na kuwaudhi wazazi wetu. Tunaomba haya katika jina lake Yesu kristo. Amen.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Luka 6:43 Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri…

Luka 6:43

Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri.Kwa
Kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake,kwa kuwa katika miiba hawachumi tini, wala katika
Michongoma hawachumi zabibu.

TAFAKARI

Matendo na nyendo za mcha Mungu yatakuwa mazuriri kila siku. Mafundisho yake na kauli
Yake vyote vitakuwa na mwelekeo wa upendo na furaha na amani. Watoto wanaokua katika nyumba ambayo haimjui wala haimchi Mungu, mara nyingi wanakua katika mazingira ya kuharibikiwa na huishia katika vyombo vya sheria. Kwa upande mwingine, neno la leo linatuambia kuwa tutatambuliwa mbele za Mungu kwa Matendo yetu maana “katika miiba hawachumi tini,wala katika michongoma hawachumi zabibu.”

SALA

Mungu baba tunakuomba utupe busara ya kuchagua ile njia nyembamba ielekeayo kwako. Utupe uwezo wa kuchagua yale mema na wewe kukutukuza milele. Maneno na mienendo yetu iwe ya kukupendeza na kukutukuza. Utujalie kwa Neema yako iliyo kubwa kupita kiasi. Amen

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Matayo 18: 19-20 Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni…

Matayo 18: 19-20

Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.

TAFAKARI

Mungu anatuhimiza sisi wanadamu tukusanyike katika nyumba za ibada au hata katika nyumba zetu na kusali pamoja. Anaendelea kusema kuwa walipokusanyika wawili au watatu naye (Mungu) yupo kati yao. Safari ya Mbinguni ni safari yenye majaribu mengi sana. Ndio sababu Mungu anasisitizia waumini kusali pamoja ili kuinuanna na kupeana moyo pamoja na kufundishana neno Lake. Ukiwa peke yako utashindwa!!!

SALA

Mwenyezi Mungu baba wa rehema,tunakushukuru kwa neno lako la leo zuri kabisa. Tunakuomba utupe moyo wa kukutana pamoja na kushirikiana katika kukutukuza wewe baba yetu uliye mbinguni. Ameen!

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Zaburi 84:5 Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake…

Zaburi 84:5

Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.

TAFAKARI

Kuna watu ambao wana vipaji mbali mbali vya kuhubiri na kufundisha neno la Mungu. Lakini kuna watu vile vile wana nguvu za ajabu na huhubiri kwa bidii lakini nguvu hizo hazitoki kwa Mungu. Ni vema wakristo wote tukamuombe Mungu ili aweze kutufunulia manabii wa ukweli na manabii wa uongo.

SALA

Tunakuja mbele zako bwana Mungu tukiomba na kushukuru kwa ufahamu mkubwa uliotupa wa kuweza kutambua mema na mabaya. Tunaomba uzidi kutufunulia uwezo wa kuweza kutofautisha nguvu za giza na nguvu toka kwako. Ameen.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Marko 11:25-26 Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu, ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu…

Marko 11:25-26

Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.
(Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.)

TAFAKARI

Tunaishi pamoja na wanadamu wenye mapungufu, ambao mara nyingi hutukwaza kwenye mambo mengi. Maaandiko yanatufundisha kusamehe saba mara sabini maana Yesu alijua kuwa kuna watu ambao wana tabia ya kurudia makosa yale yale. Ili tuweze kuishi maisha safi mbele za Mungu, inabidi tujifunze kumwomba Mungu atupe moyo wa huruma na rehema. Moyo ambao utakuwa tayari kusamehe watu wote, kuwaachilia na kutoweka kinyongo ndani ya roho zetu. Tutakapofika sehemu ambapo tutaweza kusamehe na kuendelea kuwapenda hao watu walitukosea, basi tutakuwa tumekomaa katika ukristo wetu.

SALA

Mungu wangu nisadie niweze kusamehe wenzangu kama wewe ulivyo nisamehe. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org