NENO LA LEO | Zaburi 89:7 Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka…

Zaburi 89:7

Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka.

TAFAKARI

Tunasoma katika kitabu cha Ufunuo kuwa kuna viti ishirini na vine vimezunguka kiti cha enzi, na juu ya vile viti kuna wazee ishirini na wanne, na pande zote za kile kiti cha enzi cha Mungu, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma ambao wote pamoja na wazee ishirini na wanne humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, Ufunuo 4. Kama hawa wazee ambao Biblia inasema wamevikwa mavazi maupe, na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu humsujudia Mungu mchana na usiku. Swali linakuja kwako mimi na wewe ndugu yangu, je, tunamwogopa Mungu kama itupasavyo na kumhofu kwenye maisha yetu? Je, Mungu kwetu ni nani? Tunampa nafasi katika maisha yetu au tunamchukulia kawaida sana?

SALA

Mungu wangu naomba nisamehe kwa pale niliposhindwa kuishi sawa sawa na Neno lako. Nisadie niweze kutembea kwenye hofu yako, nipe kukuogopa na kutii Neno lako kuliko kitu chochote katika maisha yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolimbus.org

NENO LA LEO | 1 Timotheo 4:10 Kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio…

1 Timotheo 4:10

Kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio.

TAFAKARI

Mungu wetu anaishi, mkono wake ni mkuu sana. Mzaburi Daudi anasema, Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kuume umetukuka, Zaburi 89:13. Mtume Paul anasema kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai. Siku ya leo nataka nikukumbushe kuwa Mungu wetu yu hai na mkono wake ni mkuu sana. Hakuna jambo linaloweza kumshinda, kinachotakiwa ni kumwendea kwa imani na utaona wokovu wake.

SALA

Mungu wangu, naweka tumaini langu kwako. Naomba uzidi kujifunua kwangu kila iwapo leo ili nipate kukufahamu zaidi. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Ayubu 22:21 Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia…

Ayubu 22:21

Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.

TAFAKARI

Mzaburi Daudi katika Zaburi 119:165 anasema, “Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.” Amani ya kweli inapatikana kwa kumjua Mungu, hapatikani kwa kuwa mkristo tu. Unaweza ukawa mkristo na hata ukasema umeokoka lakini usiwe na amani ya kweli moyoni mwako. Ukitaka amani ndani mwako inabidi umruhusu Yesu awe kiongozi wa maisha yako. Inabidi usalimishe maisha yako na kila kitu katika maisha yako mbele zake. Mpe yeye nafasi awe kiongozi wa maisha yako, mtwike mizigo yako yote na ndipo atakupa amani ipitayo fahamu zote ndani ya moyo wako.

SALA

Mungu wangu, naomba amani yako ndani ya maisha yangu. Nasalimisha kila kitu changu mikononi mwako. Nisadie niweze kukutegemea wewe siku zote. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Zaburi 90:10-12 Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini, Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara…

Zaburi 90:10-12

Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara. Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.

TAFAKARI

Kila mmoja wetu ameumbwa kwa kusudi. Hakuna ambaye ameumbwa kwa bahati mbaya. Mungu alikujua kabla hujazaliwa, Yeremia 1:5 na pia alitenga wakati maalumu utakaoishi kwenye dunia hii Esta 4:14. Mhubiri 11 inasema kila jambo na wakati wake, kuna mwanzo wa jambo na mwisho wake. Hata kipindi cha kuishi kwetu hapa duniani kimehesabiwa, kwa hiyo imetupasa kuishi maisha ya kumwogopa Mungu ili tupate kutimiza kusudi la kuumbwa kwetu.

SALA

Mungu wangu, nisadie nipate kufahamu kusudi la kuumbwa kwangu na niweze kuishi maisha yangu yote kulitimiza hilo kusudi. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK- NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 1 Petro 5:8 Muwe na kiasi na kukesha, kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze…

1 Petro 5:8

Muwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.

TAFAKARI

Kiasi ni tunda la Roho Mtakatifu, Wagalatia 5:23. Watu wengi wamejikuta wakipata hasara katika maisha kwa kukosa kiasi. Mtume Petro anatukumbusha siku ya leo kuwa tuwe na kiasi na kukesha katika maombi. Kwa kuwa mshitaki wetu Ibilisi, kama Simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Shetani hutega mitego mbali mbali ili apate kutudondosha wote dhambini. Hata leo kuna mitego yake kwa ajili yangu na yako. Tuombe Mungu atusadie tuishi na moyo wa kiasi ili tupate kuipeuka hiyo mitego na kushinda dhambi.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kuishi maisha ya kiasi. Naomba unisadie niweze kutembea na Roho wako maishani mwangu ili niweze kukua ndani yake na kuweza kuwa na matunda yake yote. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org