NENO LA LEO | Zaburi 116:12-13 Nimrudishie Bwana nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la Bwana…

Zaburi 116:12-13

Nimrudishie Bwana nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la Bwana;

TAFAKARI

Mfalme Daudi ilifika wakati katika maisha yake alitafakari ukarimu wa Bwana na akajiuliza atamrudishia Bwana nini kwa ukarimu wote alimtendea? Akaazimia kupokea kikombe cha wokovu; na kuishi maisha yake yote akilitangaza Jina la Bwana Mungu wake. Hivi ni mangapi Mungu ametutendea? Siku zote huwa tunashukuru kwa mema yote alitufanyia? Hata kama tunashukuru, je, huwa tunasimama na kuwambia wengine juu ya wema wa Mungu? Itakuwa vizuri ikifika wakati tulitangaze jina la Bwana kupitia maisha yetu ya kila siku ili Mungu apate kupewa utukufu.

SALA

Mungu wangu, asante kwa mema yote uliyonitendea. Nisadie niweze kusimulia wema wako kwa watu wengine wasio kufahamu ili wapate na wao kuonja kuwa wewe ni mwema. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Luka 6:38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa, kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu…

Luka 6:38

Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

TAFAKARI

Ukisoma vitabu vya maisha ya watu waliofanikiwa wengi wao wanasema siri moja wapo kubwa ya kufanikiwa kwao ni utoaji. Hawa ni wote wale wanaomjua Mungu na wasiomjua Mungu. Wote wanakiri walipotoa kwa moyo walijikuta milango mingi inafunguka kwa ajili yao. Hii formula ya kuwapa watu vitu Yesu alishaitoa kwenye maandiko. Alisema tuwape watu vitu, nasi tutapewa, kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachotupa vifuani mwetu. Tujifunze kutoa ndugu zangu, na kama tunataka kupokea kwa kiasi kikubwa basi nasi sisi inatubidi kutoa kwa kiasi kikubwa maana kipimo kile kile tupimacho ndicho tutakachopimiwa.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kuwa mtoaji na kusadia wale wote ambao wanahitaji msaada wangu katika maisha yao. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

2 Nyakati 7-14 Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya…

2 Nyakati 7-14

Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.

TAFAKARI

Mara nyingi tunasikia watu wa Mungu hukusanyika kwa ajili ya maombi. Kuna maombi yanajibiwa lakini mengi huwa hajibiwi. Hii haimaanishi kuwa maombi yasiyojibiwa ni magumu sana kwa Mungu ila tu ni kwamba wakati mwengine inaweza ikawa sio wakati wa Mungu kujibu au watu wake wameshindwa kufuata kanuni za maombi au ni ishara kuwa inabidi tuombe zaidi maana kuna upinzani zaidi. Tunapomwendea Mungu ni lazima tujinyenyekeze mbele zake, tuutafute uso wake huku tukiacha njia zetu mbaya. Tunapofuata kanuni hizi na huku tukiamini kuwa Mungu anaenda kujibu, tutapokea majibu ya maombi yetu sawa sawa na mapenzi ya Mungu. Nataka nikutie moyo kuwa endelea kuombea hilo hitaji lako, ipo siku Mungu atakujibu.

SALA

Mungu wangu, naleta kwako maombi ya mahitaji yangu naomba unijibu sawa sawa na mapenzi yako. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Kumbukumbu 18:9-13 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale…

Kumbukumbu 18:9-13

Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.

TAFAKARI

Kuna mambo mengi ya machukizo wakazi wa Kaanani, nchi ambayo Mungu aliwapa urithi wana wa Israel, ambayo leo inajulikana kama taifa la Israel walikuwa wanafanya. Walikuwa wanashiriki katika mambo ya kishirikina, uchawi, kuwaomba watu waliokufa kwa lugha nyingine za mizimu, kusikiliza na kufuata mapepo ya utambuzi n.k. Sijui umekutana na vitu gani vya kishirikina katika maisha yako. Leo nipo hapa kukumbusha kuwa Mungu wetu anachukizwa na kila aina ya tendo la kishirikina hata liwe dogo sana. Ukitaka uwe mkamilifu mbele zake basi kaa mbali na kila aina ya ushirikina katika maisha yako.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kutoshiriki katika aina yoyote ya ushirikina wa dunia hii. Nisadie niweze kusimama katika Neno lako siku zote za maisha yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Tito 2:11-12 Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa. Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia…

Tito 2:11-12

Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;

TAFAKARI

Maandiko yanatufundisha kuwa tumeokolewa kwa neema wala sio kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu, Waefeso 2:8-9. Hii neema iliyofunuliwa kwa wanadamu wote, inatufundisha kukataa ubaya na tama za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa katika uliwemngu huu wa sasa. Kama tunavyojua kuwa kiasi kwa lugha nyingine tunaweza sema kuishi maisha ya kujizuia, kuishi maisha ya haki ni kujitahidi kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na wanadamu wanatuzunguka, na maisha ya utauwa ni maisha ya toba au kuishi maisha matakatifu. Tukiishi hivi tunaweza shinda majaribu ya ulimwengu wetu na tutakuwa mifano bora kwenye jamii inayotuzunguka.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kuipokea neema yako na kutendea kazi katika kila jambo jema lililo funuliwa kupitia hiyo neema katika maisha yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org