NENO LA LEO | Isaya 55:6-7 Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu, Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake…

Isaya 55:6-7

Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.

TAFAKARI

Maandiko yanatutia moyo kumtafuta Bwana, maadamu anapatikana, pia kuendelea kumwita maana yu karibu au kwa maneno mengine anajibu. Inawezekana ulijaribu kumtafuta Mungu huko nyuma lakini kwa kuwa hakumwona basi ukakata tamaa na kuamua kuendelea na maisha yako. Inawezekana ulimwita kipindi fulani lakini akanyamaza na ukaona kuwa Mungu basi ni wa watu fulani na hawezi kukusikia. Kuna jambo moja inabidi ulifahamu kuwa Mungu ni mtakatifu na huwa hajichanganyi na wenye dhambi. Huwa anaweendea wenye dhambi na kuwasihi wamrudie lakini huwa ashirikiani nao kwenye dhambi zao. Kwa hiyo maadamu tunaishi kwenye mwili huu wa dhambi imetupasa kujitakasa kwanza kabla ya kwenda kutafuta uso wa Mungu. Tutapo acha njia zetu mbaya na kumrudia Bwana kwa kweli basi tutamwona na yeye atatujibu kipindi kile tutachomwita.

SALA

Mungu wangu, nisamehe kwa pale nilipoishi visivyo haki. Niwezeshe niweze acha njia zangu mbaya, na mawazo yangu mabaya nipate kukurudia wewe ili unirehemu na unisamehe kabisa. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Waefeso 4:11-12, Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii, na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu…

Waefeso 4:11-12

Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

TAFAKARI

Kuna Huduma tano za Roho Mtakatifu katika mwili wa Kristo, naposema mwili wa Kristo nina maanisha kanisa la Yesu Kristo hapa duniani. Hili kanisa si dhehebu fulani au dini fulani bali ni wale watu wote waliamua kumpa Yesu maisha yao na kumfanya awe Bwana na mwokozi wa maisha yao. Watu wanaomaani katika kazi ya msalaba wa Kristo na wanaoishi kwa kuongozwa na Roho wa Mungu. Hizi huduma zinatenda kazi hadi leo, maandiko yanasema kuwa Yesu alipofufuka alitoa wengine kuwa mitume, manabii, wainjilisti, na wengine wachungaji na waalimu. Hawa wote wapo ili wawasadie watakatifu waliopo hapa duniani kujenga mwili wa Kristo ili kazi yake ipate kwenda mbele. Ni maombi yangu Mungu azidi kuinua watu watakao kuwa tayari kufanya kazi yake katika huduma yeyote atakayo waamini nayo.

SALA

Mungu wangu, ikukupendeza naomba kwa wakati wako unitumie na mimi katika kutenda kazi katika ufalme wako. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Zaburi 118:24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia…

Zaburi 118:24

Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

TAFAKARI

Kila siku katika maisha yetu ina kusudi na faida yake. Kila siku itabaki kuwa historia na kuwa na jambo litakalo sadia kutengeneza maisha yetu ya baadaye. Kila siku Mungu anayokupa kuamka asubuhi, kwenda kufanya shughuli zako na kurudi nyumbani kwenye familia yako ni siku ya kumshukuru Mungu. Kuna wengi walilala usiku lakini hawakuamka, lakini wewe umeamka. Kuna wengi waliamka asubuhi na kwenda kwenye shughuli zao lakini hawakurudi jioni lakini wewe umepata neema ya kurudi nyumbani. Mshukuru Mungu, mtukuze kwa kukupa nafasi ya kuona siku ya leo. Jua amekuacha hadi leo maana kuna kusudi, mshukuru kwa yote katika maisha yako na endelea kumtumaini huku ukijuzua using’unike bali umshukuru katika yote. Ukiona bado unaishi basi jua Mungu bado anakusudi na maisha yako, kwa hiyo tafuta kulitimiza hilo kusudi ili ile siku upate kuvikwa lile taji utapomaliza kazi yako.

SALA

Mungu wangu, nakushukuru kwa siku ya leo. Nitie nguvu nifanye yote nayotakiwa kufanya siku hii ya leo. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Ufunuo 3:20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha. Mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami…

Ufunuo 3:20

Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

TAFAKARI

Yesu anabisha hodi kila siku kwenye maisha yetu kwa namna na jinsi tofauti tofauti. Kila siku anatuma watumishi wake waje kwetu kutuhimiza kuishi maisha matakatifu; akitamani tupate kusalimishia kila sehemu ya maisha yetu mbele zake. Kuna wengi anawasihi waache tabia fulani fulani ili wapate kufurahia wokovu wao. Kuna wengine anawaonya wapate kuacha dhambi fulani ili wapate kuwa na uzima ndani yao. Mlango wowote atakao taka aingie siku ya leo katika maisha yako, mfungulie apate kuingia.

SALA

Mungu wangu, ingia ndani mwangu na ufanyike kuwa Bwana na mwokozi wa vyote nilivyonavyo. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org