NENO LA LEO | Luka 17:6 Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii…

Luka 17:6

Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.

TAFAKARI

Kuna mambo tunakutana nayo kila siku katika maisha ambayo yanatakiwa tuwe na imani. Yesu anatufunisha kuwa tukiwa na imani kiasi cha chembe ya haradali tunaweza kuwambia mti ung’oke na ukapandwe baharini, nao utatutii. Inawezekana kuna tatizo katika maisha yako ambalo linakua kizuizi cha mipango yako. Siku ya leo nataka nikukumbushe kuwa tumia imani kama silaha ya kukusadia kulishinda hilo tatizo lako. Amini kuwa Mungu ana uwezo wa kukushindia lolote unalopitia. Amini kuwa atakuwa pamoja nawe katika njia yeyote unayopitia na mwisho wa siku utakuwa mshindi.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kusimama katika imani na kutumia imani yangu kushinda majaribu yangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | MITHALI 14:10 Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake…

MITHALI 14:10

Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake.

TAFAKARI

Mara nyingi tumejikuta tunawafariji wenzetu wanakuwa wanapitia magumu katika maisha. Ni rahisi kuona kwa njee mtu anavyoonekana ameumia lakini wakati mwengine tunashindwa kuelewa kiwango cha masumbufu ya huyo mtu ndani mwake. Maandiko yanasema moyo huujua uchungu wa nafsi yake, kwa lugha nyingine uchungu wa jambo hujulikana na yule mtu anayepitia. Kisha inaendelea wala mgeni haishiriki furaha yake, hii inaonyesha pia ni ngumu kujua namna gani mtu anaweza furahi jambo fulani katika maisha yake. Kwa kufahamu yote haya imetupasa kuwa na huruma na kujifunza kuchukuliana na watu. Kuna wengi wapo jinsi walivyo kwa sababu wana machungu mengi ndani, wengine wana historia zenye uchungu mwingi. Unaweza mwona anapendeza kwa njee na mara nyingine anaonekana amefanikiwa lakini si rahisi kuona vidonda vyake ndani. Tuombeane na kuchukuliana katika safari hii ya maisha hapa duniani.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze kuchukuliana na watu wote wananizunguka nipe kuwaombea zaidi kuliko kuwalaumu kwenye mapungufu yao nikijua kuwa nakutumikia Mungu mwenye huruma unihurumiaye kila itwapo leo. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | ZABURI 71: 1 – 3 Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe…

ZABURI 71: 1 – 3

Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe.
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.

TAFAKARI

Biblia inazungumzia kuhusu aibu ya milele(Daniel 12:2), hii ni aibu ambayo watapata watu waliishi maisha ya uovu kwenye dunia hii baada ya hukumu ya Mungu. Mara nyingi tunapoongea kuhusu mauti, hukumu na mauti ya pili kuna watu wanasikiliza kama stori tu za kutisha lakini ukweli hawatulii maanani. Mfalme Daudi aliamua kumkimbilia Bwana ili asije kuishia kuaibika milele. Alishajua kuwa kuwa kuna aibu waovu wataipata wasipotubu katika maisha haya. Kuna vifungu vingi kwenye maandiko vinavyoonyesha hili lakini kitu kimoja cha kujifunza ni kwamba ipo siku wote tutahukumiwa. Ipo siku wote tutasimama mbele za Mungu na kutoa hesabu ya makosa yetu. Tusije kuja kusahau hili, Mungu atusadie tuishi maisha ya hofu yake na kiasi ili ikifika wakati tupate kuhesabiwa haki pamoja na wale wote walio subiri ujio wa Mwana wa pendo lake ambaye ni Yesu.

SALA

Mungu wangu naomba nisadie niishi maisha ya toba. Nadondoka katika mambo mengi na nakosea kwenye mengi. Nipe kutubu kwa pale napokosea ili niweze tembea kwenye neema yako. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Wagalatia 2:9 Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara…

Wagalatia 2:9

Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara.

TAFAKARI

Yakobo, Kefa ambaye ni Petro na Yohana walikuwa ni mitume walikuwa pamoja na Yesu. Walipoona neema ilikuwa katika maisha ya Paulo na Barnaba waliwapa mkono wa kuume washirika kama ishara kuwa wametambua huduma yao na wakawaruhusu kwenda kuuhubiri Injili kwa mataifa. Tuna vurugu nyingi sana katika kanisa la leo kwa sababu kuna watu walimpokea Roho Mtakatifu na wakajua mistari miwili mitatu na hujiona kuwa wanafaa kuwa watumishi na kutafuta nafasi za kutumika hata kama kwa lazima. Ni mapenzi ya Mungu wote tuokolewe na tuufikie ule uzima, lakini sio kusudi lake wote tuwe waalimu wa Neno lake kama Yakobo 3:1 inavyosema, “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.” Kama kuna mambo au jambo bado hujapata neema ya kulielewa basi ni hekima ukanyamaza kuliko kutoka na kufundisha tofauti na kuishia kupotosha kanisa. Mungu atusadie tuweze kuwa wapole na wenyenyekevu katika mambo yote yanayohusu kumtumikia.

SALA

Mungu wangu, nisadie niweze simama kwenye wito wangu. Nisije lazimisha kufanya kitu ambacho Mungu hukukusudia nifanye kwenye kanisa lako. Bali nipe neema ya kujua na kutembea kwenye kusudi lako. Kwa Jina Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 2 Wafalme 5:10-11 Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi…

2 Wafalme 5:10-11

Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. 11. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma.

TAFAKARI

Naamani alikuwa jemadari(commander) wa jeshi la Waashamu ambao kwa lugha nyingine ni Wasyria. Huyu jamaa alikuwa na ukoma, alikuwa ni tajiri na kila kitu ambacho nafsi yake ilikuwa inatamani. Aliposikia kuwa kuna nabii katika Israel aitwaye Elisha ambaye angeweza kumponya ukoma wake. Akafunga safari lakini hakutaka kufuata maelekezo ya nabii lakini alitaka nabii amponye huko ugonjwa wake kama atakavyo yeye. Wakati mwengine katika maisha tunakuwa na jambo ambalo limetushika na linaweza kuwa ndo ukoma wetu. Kila watumishi wa Mungu wanapotuambia tufanye vitu fulani fulani na kuacha vingine ili tupate miujiza yetu huwa tunadharau. Matokeo yake ukoma wetu unabaki na tunaendelea kutembea kwenye shida zetu. Mwisho wa siku Naamani alikubali na akapokea muujiza wake. Siku ya leo nakusikii na wewe kubali unachoambiwa na watu wa Mungu ili upate upenyo(breakthrough) wako pia.

SALA

Mungu wangu, naomba niondolee ubishi ndani yangu. Niumbie moyo wa kutii maagizo ya watumishi uliwaweka katika maisha yangu ili nipate kustawi na kufanikiwa. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK_Neno
www.iykcolumbus.org