NENO LA LEO | Luka 15:4 Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone…

Luka 15:4
Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?

TAFAKARI

Yesu ndiye mchungaji mwema na sisi ni kondoo zake. Kwa mfano huu Yesu anaonyesha upendo wake aliokuwa nao kwetu sisi wanadamu kiasi kwamba hawezi kukubali hata mmoja wetu apotee. Mafarisayo walimshutumu Yesu kuwa anakula na wenye dhambi na ndio maana akatoa mfano huu wa mchungaji mwema na
kondoo. Yesu alikuja kwa ajili ya wenye dhambi na kila mmoja wetu atakayempokea atapata uzima wa milele.

SALA

Hasante Mungu kwa siku nyingine tena uliyotupa iliyojaa furaha na amani. Hasante kwa neno lako la leo Zuri.Tunapata faraja kila tunapokumbuka upendo wako kwetu sisi binadamu. Tunaomba uzidi kutubariki siku zetu zote za maisha hapa duniani. Amen

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Wagalatia 6:8 Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele…

Wagalatia 6:8
Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

TAFAKARI

Binadamu tunaanguka kwenye dhambi kwa sababu ya kushindwa kuhimili matakwa ya miili yetu. Tunashindwa kutawala miili yetu na kuwa dhaifu katika maamuzi. Kila mara roho huwa inatuelekeza katika njia sahihi lakini tunashindwa kufuata ile sauti ndogo ya roho inayotuonya na tunafuata matakwa ya miili yetu. Yeyote anayetii ya kimwili atavuna uharibifu,bali yeye anayeitii roho atavuna uzima wa milele.

SALA

Mungu baba wa rehema, tumekukosea mara nyingi sana tukastahili adhabu yako lakini kwa neema yako iliyo kuu umetusamehe. Tunakuomba utupe ujasiri wa kuchunga matakwa ya miili yetu ili tufanye tu yale yanayokupendeza. Amen

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Mathayo 16:24 Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate…

Mathayo 16:24
Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

TAFAKARI

Kuna tofauti kati ya kusema mtu anataka kumfuata Yesu na kukubali kumfuata Yesu. Njia iendayo kwa yesu ni nyembamba na yenye kona nyingi sana. Wengi wanaanza safari ya Kumfuata Yesu vizuri lakini wanaishia njiani. Yesu anasema kuwa pamoja na kuwa njia ni nyembamba, kuna msalaba wa kubeba na kujikana nafsi yako kabla ya kuongozana naye.Ndugu zangu tujipe moyo na tusali sana ili tusishindwe safari hii ya kumfuata Bwana Yesu

SALA

Mwenyezi Mungu, baba yetu tunakuomba utuongoze hapa duniani katika hii safari yetu ya kuja kwako. Utusaidie pale tunapolemewa na misalaba yetu. Tunaomba haya katika jina lake Yesu Kristo. Amen

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Mithali 14:23-24 Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu. Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu…

Mithali 14:23-24
Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu. Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.

TAFAKARI

Kuna kundi kubwa la watu ambao kila siku wana mipango ya kutafuta pesa na bisahara kubwa kubwa.Kila mara unapokutana nao wanakuelezea mipango yao hiyo lakini hela mfukoni hawana kabisa.Leo Bibilia inawaonya na kuwambia kuwa wakafanye kazi waache porojo! Maneno matupu huleta hasara.Taji ya mwenye hekima ni mali zako.

SALA

Mwenyezi Mungu baba wa rehema, tunakushukuru kwa hii siku mpya uliyotupa. Tunakuomba uzibariki kazi za mikono yetu ili kila tutakachogusa kigeuke kuwa mafanikio. Tunaomba haya katika jina la mwokozi wetu Yesu kristo, Amen.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Matayo 18: 19-20 Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni…

Matayo 18: 19-20
Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.

TAFAKARI

Mungu anatuhimiza sisi wanadamu tukusanyike katika nyumba za ibada au hata katika nyumba zetu na kusali pamoja. Anaendelea kusema kuwa walipokusanyika wawili au watatu naye (Mungu) yupo kati yao. Safari ya Mbinguni ni safari yenye majaribu mengi sana. Ndio sababu Mungu anasisitizia waumini kusali pamoja ili kuinuanna na kupeana moyo pamoja na kufundishana neno Lake. Ukiwa peke yako utashindwa!!!

SALA

Mwenyezi Mungu baba wa rehema,tunakushukuru kwa neno lako la leo zuri kabisa. Tunakuomba utupe moyo wa kukutana pamoja na kushirikiana katika kukutukuza wewe baba yetu uliye mbinguni. Ameen!

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org