NENO LA LEO | Zaburi 84:5 Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake…

Zaburi 84:5

Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake

TAFAKARI
Kuna watu ambao wana vipaji mbali mbali vya kuhubiri na kufundisha neno la Mungu. Lakini kuna watu vile vile wana nguvu za ajabu na huhubiri kwa bidii lakini nguvu hizo hazitoki kwa Mungu. Ni vema wakristo wote tukamuombe Mungu ili aweze kutufunulia manabii wa ukweli na manabii wa uongo.

SALA
Tunakuja mbele zako bwana Mungu tukiomba na kushukuru kwa ufahamu mkubwa uliotupa wa kuweza kutambua mema na mabaya. Tunaomba uzidi kutufunulia uwezo wa kuweza kutofautisha nguvu za giza na nguvu toka kwako. Ameen!

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Mithali 23 : 22-25 Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee. Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu…

Mithali 23 : 22-25
Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee. Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu. Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia. Na wafurahi baba yako na mama yako; Na afurahi aliyekuzaa.
TAFAKARI
Bila ya wazazi wetu, tusingalikuwepo hapa duniani. Mtu anayewazarau wazazi wake hawezi kupata thawabu mbele ya mwenyezi Mungu. Huwezi kujidai kuwa unampenda Mungu huku unawazarau wazazi wako. Neno linatuagiza kuwasikiliza na kuwapenda wazazi wetu muda wao wote hapa duniani.Furaha ya wazazi wetu ndio mafanikio yetu!
SALA
Tunakushukuru Mungu wetu kwa Baraka ya wazazi uliotupa. Tunakuomba utusamehe pale tunapotetereka na kuwaudhi wazazi wetu. Tunaomba haya katika jina lake Yesu kristo. Amen.
©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Mithali 4: 20-27 Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu…

Mithali 4: 20-27
Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.
Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe. Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.

TAFAKARI

Katika maisha mafundisho na maonyo tupatayo toka kwa wazazi na waliotutangulia kiumri ni muhimu sana. Katika somo la leo tunaonywa kulinda moyo wetu kuliko vitu vyote tunavyovilinda. Hii ni kwa sababu mambo yote huanzia moyoni. Mema yote na mazuri yote yanakaa mioyoni mwetu. Basi tukampe bwana Yesu mioyo yetu ili aisafishe na kuilinda.

SALA

Mwenyezi Mungu baba wa rehema, tunaikabidhi mioyo yetu kwako uipe unyenyekevu na upendo kwa watu wote. Tunaomba haya katika jina la bwana wetu Yesu kristo. Amen
©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Warumi 5:8 Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu…

Warumi 5:8
Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
TAFAKARI

Waandishi wa Agano Jipya wametumia maneno matatu ya kiyuyani kuelezea aina za neno UPENDO. Neno la kwanza ni Philia, lenye maana ya upendo wa kirafiki. Neno la pili ni eros, lenye maana ya upendo uliojengwa katika misingi yenye kutamani. Aina hizi mbili za upendo zina misingi ya masharti. Masharti yenyewe ni mwenye kupenda anao uwezo au uhuru wa kuamua kutokupenda. Kwa mfano, ni hali ya kawaida kabisa kusikia mtu akisema, kuanzia leo mimi na wewe basi. SIKUPENDI tena! Upendo huu ni wa kibinadamu. Aina hizi mbili, zinatuangusha tulio wengi. Eros ni pendo la chuki.
Aina ya tatu ni ya upendo ni wa AGAPE. Agape ni upendo uliojengwa katika misingi ya upendo wa dhati. Agape ni upendo wa kweli. Agape ni upendo usio wa unafiki ndani yake. Agape ni upendo wa Kimungu. Somo la leo linatukumbusha kwamba, Mungu anatupenda kupita upeo. Upendo wa Mungu kwetu hauna kifani. “Tulipokuwa wenye dhambi,” Mungu alimtuma Yesu Kristo aje atuokoe. Huu ndio upendo wa dhati. Upendo wa Agape! Mimi na wewe, tunakumbushwa kumuomba Mungu atuondolee pendo la eros. Naam, atuondolee upendo wa philia. Mungu mwingi wa Agape, anao uwezo wa kutosha kutusaidia ili tuwe na upendo wa kweli. Upendo wenye kuleta umoja. Upendo wenye kuondoa chuki. Upendo wenye kuleta amani. Agape! Palipo na agape yote yanawezekana. Mungu na atusiadie, ili 2017 uwe ni mwaka wa Agape. Amina.
SALA

Mungu wa Agape, tunakushukuru kwa kutupenda sisi wenye dhambi. Tunakuomba utupe uwezo wa kukupenda Wewe na kuwapenda na wenzetu, Amina
©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org