NENO LA LEO | 1 Samweli 3: 13-14 Kwa maana nimemwambia (Eli) ya kwamba, nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia…

1 Samweli 3; 13-14

Kwa maana nimemwambia (Eli) ya kwamba,nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua:kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia. Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli,ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafishika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.

TAFAKARI

Eli alikuwa mcha Mungu na Kuhani mkuu katika Hekalu la Bwana. Eli alikuwa na watoto wawili Hofni na Fineasi. Sifa mbaya za hawa wototo zilienea katika mji walipoishi. Walikuwa wananyanyasa waumini wakienda kuabudu na kutoa sadaka. Baba yao Eli alijua habari hizo za sifa mbaya za watoto wake lakini hakufanya lolote kuwazuia. Hiki kitendo cha kutowazuia watoto wake kutenda maovu kilimchukiza sana Mungu. Ndipo Mungu kupitia kwa mtumishi wake Samweli akatoa adhabu kali sana kwa Eli na familia yake.

Mara nyingi wazazi wanashindwa kuwalea watoto wao katika njia ambazo zinampendeza Mungu. Wanawaachia watoto wanakuwa vituko, wanakuwa wezi, wanakuwa hawaheshimu watu. Maandiko matakatifu katika kitabu hiki cha samweli wa kwanza yanatuonya kwamba hukumu ya Mungu itatuangukia sisi wazazi pamoja na watoto wetu kama hatutachukua hatua zinazostahili kurekebisha watoto wetu. Wazazi wengi wanashindwa kuwarekebisha watoto wao tangu wakiwa wadogo, kitu ambacho kinapelekea kuwa vigumu sana kuwarekebisha wakishakuwa wakubwa. Ukiendelea kusoma mistari ya mbele katika kitabu hiki cha 1 samweli utakuta kuwa Hofni na Fineasi waliuawa siku moja wote wawili na baba yao Eli alifariki baadaye. Wazazi hamtaweza kujitenga na uovu wa vizazi vyenu. Ni vema kumuomba Mungu aibariki familia ya kila mmoja wetu ili nyumba zetu zikuwe katika mazingira ya kumpenda bwana Yesu. Luka 6:43, Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya,wala mti mbaya uzaao matunda mazuri.

TUOMBE

Mwenyezi Mungu tunakuja kwako na watoto wetu na wazazi wetu na vyote vilivyo ndani ya nyumba zetu. Tunakuomba utupe busara za kuweza kuwalea watoto wetu katika mwenendo wa kukupenda na kukutumikia wewe. Utusamehe pale tunapokosea. Roho wako mtakatifu akae ndani yetu Milele. Amen.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Mwanzo 22:13-14, Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka…

Mwanzo 22:13-14

Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,kama watu wasemavyo hata leo,Katika mlima wa BWANA itapatikana.

TAFAKARI

Maana ya neno Yehova-Yire ni kwamba Bwana atatoa, au Bwana atatupa. Ibrahim alipotaka kumtoa sadaka mwana wake wa pekee Isaka, Mungu alimpa mwana kondoo ili afe badala yake. Hii ikiwa inaonyesha kwa namna gani Yesu kama mwana kondoo wa Mungu atakufa kwa dhambi za wanadamu. Hili neno lina maana pia kuwa Mungu atatupatia mahitaji yetu yote tunayohitaji kwa wakati tunayohitaji. Ni moja Kati ya majina ya Mungu, Yehova-Yire, ambalo watu wa Mungu wanatumia katika maombi yao kumkumbusha Mungu ili apate kukutana na mahitaji yao. Leo unaweza kumwomba Yehova-Yire apate kutana na mahitaji yako na kukupa haja za moyo wako.

SALA

Mungu wangu na Baba yangu, naomba kutana na mahitaji yangu siku ya leo. Upate kutimiza haja zote za moyo wangu sawa sawa na mapenzi yako kwangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 2 TIMOTHEO 2:19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake…

2 TIMOTHEO 2:19

Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama,wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena,Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.

TAFAKARI

Tunaona Mungu wetu anasema anawajua walio wake Kwa sababu yeye ni Mungu na ndiye aliye tuumba.Jinsi tulivyo ni kwa mapenzi yake.Ila wenye kutenda mema na maagizo yake ndiyo watakao ungana naye kule PARADISO siku ya mwisho.Mungu anaendelea kutuambia katika neno lake kuwa YEYOTE anayelitaja jina lake basi HANA BUDI kuuacha UOVU.Mpendwa mtu wa Mungu,hapo uliko,inawezekana umekuwa ukiwa na mahudhurio mazuri kanisani,ukitoa zaka zako kwa uaminifu.Swali linakuja,je,umeuacha UOVU?.Ni lazima tuuche uovu ili tuweze kuingia paradiso(MBINGUNI).

SALA

Mungu mwema,asante tena kwa siku ya leo.Umependezwa na sisi kulisikia tena hili la uzima.Sasa tunajua kuwa ni lazima tuache uovu ili tuingie mbinguni.Hivyo Mungu wetu ingia katika akili ulizotupa na kutufanya tuelewe na kutii maandiko yako matakatifu.Tunakuomba utufanye tuwe imara katika kukutegemea wewe tu.Ni katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo tumeomba.Amen.

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | WARUMI 1:28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyo wapasa…

WARUMI 1:28

Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao,Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa,wayafanye yasiyo wapasa.

TAFAKARI

Tunaona jinsi ambavyo watu wa Mungu tunapoacha kutenda yale ambayo Mungu ameyaagiza,matokeo yake Mungu hutuacha,na anapo tuacha hatma yake ni kwamba huwa tunaangukia kwenye kutenda yasiyo tupasa(DHAMBI),na sababu ya msingi ya sisi kutenda dhambi ni kwasababu huwa tunaacha kutumia akili alizotupa Mungu na kuanza kutumia akili zetu,ambazo HAZIFAI.Watu wa Mungu tuna kila sababu ya kumgeukia Mungu kwani hata kukosa kwetu mafanikio ni Kwa sababu ya akili zetu zisizofaa,ambazo zimeletwa na kuishi nje ya mpango wa Mungu.Tukitaka kubarikiwa ni LAZIMA tutende yanayo mpendeza Mungu na kumtafuta Mungu kwa BIDII.

SALA

Eee Mungu wetu,uliye mwema sana.Neno lako ni taa na nuru katika maisha yetu.Asante kwa kutuletea hili neno.Ni zuri sana na lenye kutubariki.Tunakuomba ufungue ufahamu wetu ili hili neno liyabadili maisha yetu kwani walio wengi hatujui kuwa tunaishi kwa kufuata akili zetu,ambazo hazifai.Tunahitaji kutumia akili ulizo tubariki nazo kwa kukutegemea wewe tu milele.Ni katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo,tumeomba.Amen

©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org