NENO LA LEO | Waebrania 10:38-39 Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani…

Waebrania 10:38-39
Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.
Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.

TAFAKARI

Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana, Waebrania 11:1. Maandiko yanatufundisha juu ya kuishi maisha ya imani. Katika maisha yetu ya kila siku hali halisi huwa inapingana na yale mambo tunayotamani yatokee katika maisha. Inawezekana unatamani mtoto lakini madaktari wamesema huna uwezo wa kuzaa. Inawezekana unatamani mume lakini unaona umri wako umeenda sana na huna imani kama anaweza akatokea mtu atakaye kuoa. Pia inawezekana unaumwa ugonjwa fulani ambao hauna dawa na umepoteza tumaini lako la kuishi. Au inawezekana unatamani ukasome kitu fulani ambacho kinaweza kukupa kazi nzuri baadaye lakini huna uwezo na majukumu yamekuzunguka.

Sijui ni jambo gani ambalo linaonekana haliwezekani kwako lakini maandiko yanatufundisha kuwa yote yawezekana kwa yule aaminiye, Marko 9:23. Leo nimekuja hapa kukutia moyo kuwa mwamini Mungu, amini kuwa yeye anaweza kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu, Waefeso 3:20. Amini kuwa sio mwisho wa njia yako mpaka pale Mungu atakaposema umefika mwisho. Kama bado unapumua basi jua lipo tumaini, siku moja utaitwa mama, ipo siku utaolewa, ipo siku Mungu atakuponya na ipo siku utasoma na kupata kazi nzuri. Endelea kumwamini Mungu.

SALA

Mungu wangu ninakuamini siku ya leo. Naamini kuwa hujaniacha, naamini kuwa upo na mimi. Naamini kuwa unaenda kunitendea muujiza wangu na mimi nitakutukuza mbele za watu wote. Kwa Jina la Yesu, Amina.
© IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Wafilipi 4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

Wafilipi 4:13
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

TAFAKARI

Kuna vipindi tofauti katika maisha.Vipindi vingine mambo yanaenda vizuri lakini kuna vipindi vingine mambo yanakuwa si mazuri kabisa. Kuna wakati tunajikuta tuna pesa na wakati mwingine tunakuwa hatuna. Kuna vipindi vingi katika maisha, lakini katika vipindi vyote tunahitaji nguvu ya Mungu kutusadia kushinda. Katika kipindi chochote unachopitia wakati huu napenda ufahamu kuwa yupo Mungu anayeweza kukutia nguvu. Yupo Mungu ambaye anaweza kukushindia majaribu na kukusadia upate ufahamu unaouhitaji ili uweze kufanikiwa katika maisha haya.

SALA

Mungu wangu, naomba unitie nguvu siku hii ya leo. Nisadie niweze fanya yote sawa Sawa na mpango wako maishani mwangu. Kwa Jina la Yesu, Amina.
©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Kumbukumbu 8:18-18 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo…

Kumbukumbu 8:18-18
Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo.
Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.

TAFAKARI:

Kila nikikumbuka kule Mungu aliponitoa napata sababu ya kumshukuru na kuendelea kumwogopa Mungu daima. Sijui kuhusu wewe ndugu lakini kuna pahala Mungu amenitoa na nipo nilivyo leo kwa ajili ya neema na rehema zake maishani mwangu. Mara nyingi tunapopata elimu, mali, wame, wake, watoto au hata vyeo kwenye jamii huwa tunasahau pahala Mungu alipotutoa. Wengi wetu tunajikuta tunaanza kuishi maisha ya kuigiza kana kwamba vitu tulivyo navyo leo vilikwepo toka pindi tulipozaliwa. Unakumbuka kile kipindi ulichokuwa unamlilia Mungu akupe hayo maisha uliyo nayo leo? Sasa mbona leo unaishi maisha ya majivuno na kujikinai? Hujui ni neema ya Mungu na mkono wake ndio umekutendea makuu?

Nakusihi ukumbuke Mungu alipokutoa asubuhi ya leo, kumbuka kuwa kuna wakati hukuwa na vitu ulivyonavyo leo. Kama ulinyenyekea wakati ule na Mungu akakuinua mpaka hapo ulipo; hujui kuwa ukinyenyekea wakati huu Mungu atakufanyia mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.(1 Wakorintho 2:9)

SALA

Mungu wangu nisamehe kwa pale niliposahau mahala nilipotoka. Nisadie niweze kuishi maisha ya unyenyekevu na kujishusha nikijua nipo jinsi nilivyo leo kwa neema yako tu. kwa Jina la Yesu, Amina.
©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Waefeso 5:20 Wakati wote na kwa kila kitu mshukuruni Mungu…

Waefeso 5:20
Wakati wote na kwa kila kitu mshukuruni Mungu Baba katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

TAFAKARI

Ni rahisi kumshukuru Mungu pindi mambo yanapokuwa mazuri, wakati kuna amani kwenye nyumba yako, watoto wako wazima na una uwezo wa kukutana na mahitaji yako ya kila siku. Hapa wengi wetu huwa tunamrudishia sifa Mungu kwa moyo mkunjufu. Pindi mambo yanapoanza kuwa magumu, tunapoanza kupambana na magonjwa na majaribu ya kiuchumi roho zetu zinaanza kuzimia ndani yetu. Sijui unapitia kipindi gani cha maisha sasa, lakini nipo hapa kukumbusha na kukutia moyo kuwa mshukuru Mungu kwa hali unayopitia. Mshukuru Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuru Mungu kwa magumu yote katika maisha yako, huku ukikumbuka katika kila jaribu ambalo unapitia Mungu huwa anaweka mlango wa kutokea ili uweze kustahimili.

SALA

Mungu wangu, nakushukuru kwa zawadi ya maisha. Asante kwa yote ambayo umenipa na ambayo hujaruhusu nipate kwenye maisha yangu. Najua una mpango mzuri na mimi, naomba uzidi kunipigania na kunisadia. Kwa Jina la Yesu, Amina.

©IYK-NENO

www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Yeremia 29:11Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi…

Yeremia 29:11

Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.

TAFAKARI

Neno tumaini siku zenu za mwisho, katika lugha ya kigeni linaweza tafsiriwa kama: “To give you an expected end, wengine wametafsiri kama to give you hope in your final outcome, au to give you future and a hope.” Nabii Yeremia Kama alivyojulikana alikuwa nabii wa maombolezo(a weeping prophet).Siku ya leo anakuja na Neno la faraja kwetu sisi. Kwamba Mungu anajua mawazo anayotuwazia; na ni mawazo ya amani wala si ya mabaya. Hili linafuta yale mawazo yote kuwa Mungu anakuchukia au Mungu amekuchoka! Inawezekana umefanya mambo kadhaa ambayo yamekufanya uogope hata kumsogelea Mungu; maana unadhani Mungu ana chuki na wewe.

Neno lake siku ya leo linasema Mungu hana chuki na wewe bali anakuwazia mawazo ya amani wala si mabaya. Anachukia zile dhambi zote ulizofanya au unazofanya lakini anakupenda wewe upeo. Lengo lake ni kukupa wewe “an expected end”.Kwa lugha nyingine kukufikisha kule ambapo roho yako inatamani kufika kabla hujarudi kwake. Anataka wewe ufikie ndoto zako na utimize kusudi la kuumbwa kwako. Nakusihi mfungulie moyo wako siku ya leo ili apate kuingia na kutawala.

SALA

Mungu wangu na Baba yangu, nimefanya mengi ambayo yameninyima ujasiri kuja mbele zako. Mara nyingi nimehisi kama upo mbali wakati upo karibu kuliko hata pumzi yangu. Naomba nisamehe na ninatamani ukaribu na wewe mara nyingine tena. Kwa Jina la Yesu, Amina.
© IYK-NENO
www.iykcolumbus.org