NENO LA LEO | 1 Wakorintho 15:52-53 Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho…

1 Wakorintho 15:52-53
Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.  Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

TAFAKARI:

Kila mmoja wetu kwa nyakati tofauti katika maisha haya tumejikuta tunapoteza watu tulio wapenda. Kila mara tunapokumbuka wale wote ambao mauti imewachukua huwa tunaumia na wakati mwengine inaonekana kama sio kweli. Maandiko yanatufundisha juu ya ufufuo wa wafu, kuwa ndani ya Yesu kuna kufufuliwa baada ya maisha haya. Hili limeandikwa kutupa tumaini kwamba hatupigi mbio bure kwenye huduma yetu ndani ya Kristo Yesu. Hii inatufundisha kwamba siku moja tutakuja kuwaona na kukutana na ndugu zetu wote waliokufa katika Bwana. Pia inatuhimiza sisi tulio hali kuendelea kusimama imara katika imani tukijua kuwa kazi yetu si bure katika Bwana.

SALA:

Mungu wangu nakushukuru kwa maisha ya wale wote walio nitangulia. Asante kwa muda ulionipa kuwa nao. Naomba uzidi kunitia nguvu huku Roho wako Mtakatifu akinifariji kila mara napowakumbuka nikijua siku moja nitakuja kuwaona tena ndani yako. Kwa Jina la Yesu, Amina.
©IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | 2 Wakorintho 2:9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu

2 Wakorintho 2:9

Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

TAFAKARI:

Kila mmoja wetu ana udhaifu fulani. Wote tuna vijitabia na wakati mwengine tuna misimamo ambayo inaonyesha udhaifu wetu mbele za wenzetu. Kuna watu wana madhaifu ambayo yanavumilika lakini wengine yanakuwa yanashindikana kuvumilika na baadhi ya watu ambayo inapelekea hao watu kukataliwa. Inawezekana watu wanakukataa kwa sababu ya madhaifu yako, watu wengi wanakuona hufai maana kuna shida wanaiona maishani mwako.
Leo nina habari njema juu yako, kuwa neema ya Mungu inakutosha; maana uweza wa Mungu hutimilika katika udhaifu. Salimisha madhaifu yako mbele za Mungu. Mwambie ni wapi huwezi, mwambie ni tabia gani zinakushinda. Mungu wetu hatakukata Kama wengine walivyofanya. Mzaburi Daudi anasema, Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake, Zaburi 27:10. Yesu yupo tayari kukukaribisha nenda kwake leo kwa imani, naye akusadia ushinde madhaifu yako.

SALA:

Mungu wangu naleta madhaifu yangu mbele zako. Nisadie niweze kuyashinda na kuishi maisha matakatifu ya kukupendeza. Kwa Jina la Yesu, Amina.
(C)IYK-NENO
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO | Yoshua 1:3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.

Yoshua 1:3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.

TAFAKARI: Maandiko yanatufundisha kuwa Mbingu ni Nchi ni mali ya Bwana. Tena yanasema mbinguni ni kwake Mungu lakini nchi amewapa wanadamu waishi; kisha Fedha na dhahabu yote pia ni mali yake.
(Zaburi 24:1,115:16, Hagai 2:8)
Kwa kuwa vyote ni vya kwake, alimpa Abraham urithi wa nchi ili iwe yake yeye na vizazi vyake hata milele. Leo hii Mungu amekuweka wewe kwenye hii nchi kwa kusudi. Leo hii ungeweza kuwa pahala popote duniani lakini upo hapa maana Mungu ameamuru uwepo. Nataka nikutie moyo kuwa usiogope ndugu yangu. Mwamini Mungu katika yote ufanyayo. Naamini kwa moyo wangu wote Mungu anataka ufanikiwe, Mungu anataka uwe na afya njema na maisha mazuri. Kama unapambana bado na shida, siku ya leo liite Jina la Bwana Mungu wako. Mkumbushe akupe ile baraka aliyokuandalia katika nchi hii. Hata kama unaona umebarikiwa katika maeneo mengi basi usiache kumwita akutembelee katika maeneo yale yote uliyopungukiwa.

SALA: Mungu wangu, kutana na mahitaji yangu siku ya leo. Naomba uje upate kufuta yale machozi yangu ya sirini. Kutana na ile haja ya moyo wangu ili nipate kukutukuza wewe daima. kwa Jina la Yesu nimeomba,  Amina.
(c)IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO: Zaburi 109: 1-5 Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze,. . .

NENO LA LEO: Zaburi 109: 1-5 Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze, Kwa maana wamenifumbulia kinywa; Kinywa cha mtu asiye haki, cha hila, Wamesema nami kwa ulimi wa uongo. 
Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka, Wamepigana nami bure.Badala ya upendo wangu wao hunishitaki, Ijapokuwa naliwaombea. Wamenichukuza mabaya badala ya mema, Na chuki badala ya upendo wangu. 
TAFAKARI:Wakati mwingine binadamu watakulipa mabaya japokuwa wewe unawatendea mema. Watakusengenya na kutaka kukuharibia maisha yako kabisa pamoja na kwamba uliwasaidia. Wakati mwingine inakuwa ni wivu tu na wakati mwingine inakuwa ni chuki tu zisizo na msingi wowote. Mwimba zaburi anatufundisha kuwa kwa Mungu hakuna linaloshindikana. Hivyo kila mara tunapokuwa katika matatizo tumlilie Mungu. Tumuite Mungu naye atatuitika (yeremiah 33:3)
SALA: Baba Mungu tunakuita utusimamie katika safari yetu hapa duniani kwa sababu shetani haishi kutuingilia watumishi wako na kutaka kututenganisha sisi na wewe. Utulinde ili maadui zetu wajue kuwa sisi tunamtumaini Mungu aliye hai ambaye kwake hakuna linaloshindikana. AMEN!
(c)IYK_Neno