NENO LA LEO: Mwanzo 3:12 – 13 Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo…

NENO LA LEO: Mwanzo 3:12 – 13 Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.

TAFAKARI: Mungu wetu SIYO Mungu wa LAWAMA.  Tangu mwanzoni, MWANADAMU alipoamua kuisikiliza SAUTI ya shetani, dhambi ya
LAWAMA iliyatawala maisha yake.  Somo la leo, linamshuhudia baba yetu Adamu, anavyomlaumu MUNGU. “…huyu MWANAMKE uliyenipa …ndiye aliyenipa MATUNDA ya mti huo, NIKALA.  Mama yetu Eva, kama vile Adamu, naye AKAMLAUMU, nyoka “ …nyoka alinidanganya, NIKALA.”
Matokeo ya dhambi ya LAWAMA ni ADHABU ya MAUTI.  Dhambi hii imeendelea kukisumbua hata kizazi cha leo.  Mungu wetu hafurahishwi na LAWAMA zetu. Kwa MOYO wa UPOLE na kwa MACHOZI yenye HURUMA, Mungu aliamua kutufia juu ya MSALABA. Msalaba unaoturudisha ndani
ya EDENI mpya; yaani, maisha ya WOKOVU! Msalaba huu, unatuokoa dhidi ya nguvu ya DHAMBI, KIFO, na SHETANI, amina.

SALA: Ee Mungu wetu, tunakuomba utupe nguvu ya kumshinda shetani na kazi zake zote.  Utusaidie ili tuyatende mapenzi yako
maishani mwetu, ni katika Jina la Yesu Kristo, Amina .
(c)IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO: Zaburi 99:6-8, Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake,

NENO LA LEO:  Zaburi 99:6-8, Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia; Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao. Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa. Ee Bwana, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu; Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe Ingawa uliwapatiliza matendo yao.
TAFAKARI: Mungu wetu ni Mungu mwenye kusamehe. Kila itwapo leo hutuma watumishi wake katika kila kona ya ulimwengu kwa namna tofauti tofauti wapate kufikisha huu ujumbe wa msahama kwa wanadamu. Huyu Mungu hajaanza leo kusamehe, alifanya hivyo hata kipindi cha Agano la kale na aliwasamehe watumishi wake na watu wote walimwendea kwake wakiwa na moyo wa toba. Kuna wengi wanadhani kuwa dhambi na maovu yao ni mengi kiasi ambacho Mungu hawezi kuwasamehe. Wanafikiri kuwa Mungu anawachukia na hawezi tena kuwarehemu. Maandiko yapo wazi kuwa dhambi zetu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama bendera, zitapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu kama tutazitubu, Isaya 1:18. Nakusihi uende mbele za Mungu na ukatubu kwa pale ambapo una shuhudiwa ndani ya moyo wako kufanya hivyo. Mungu ni mwenye huruma na atakusamehe kabisa.
SALA: Mungu wangu, naomba nisamehe kwa dhambi na maovu yangu yote. Futa jina langu katika kitabu cha hukumu na liandike kwa upya kwenye kitabu cha hukumu. Kwa Jina la Yesu, Amina.
(c)IYK_Neno
www.iykcolumbus.org

NENO LA LEO: Yohana 14:12, Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, . . .

NENO LA LEO: Yohana 14:12, Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.

TAFAKARI: Kanisa la kwanza lilisimamia haya maneno ya Yesu na si ajabu ndo maana walitembea katika ushindi huku wakidumu kwenye furaha ya Roho Mtakatifu siku zote. Naamini zimefika nyakati kwa kanisa la Yesu Kristo la wakati huu kurudi kwenye maandiko na kuanza kusimamia ahadi zake. Naamini ni wakati ambao Ukristo wetu usibaki kwenye maandishi na viapo tu bali uwekwe kwenye matendo na kumpa Mungu nafasi ya kukutumia. Naamini kuwa kila mmoja wetu anaweza kutumiwa na Mungu kwa namna ya ajabu na kufanya mambo makubwa kama Yesu alivyo ahidi. Tatizo halipo kwa Mungu, wala si shetani bali tatizo kubwa la maendeleo ya Mkristo ni yeye mwenyewe. Ifike wakati mtu wa Mungu ukubali kuachana na huu ulimwengu ulio lewa maovu na unaosusua karibia kuanguka na umpe nafasi Mungu akutumie. Ukimpa nafasi basi uwe na hakika shetani na jeshi lake lote la kuzimu hataweza zuia wito wa Mungu ndani mwako ufanye kazi.

SALA: Mungu wangu, naomba nitumie katika kujenga ufalme wako. Natamani kuona mkono wako ukitenda kazi kupitia maisha yangu; natamani kuona ukinitumia niwe chombo cha mabadiliko katika jamii yangu. Nakupa sifa maana ahadi zako ni kweli na amina, Kwa Jina la Yesu, Amina.
(c)IYK_Neno

NENO LA LEO: Zaburi 118:24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia. . .

NENO LA LEO: Zaburi 118:24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

TAFAKARI: Kila siku katika maisha yetu ina kusudi na faida yake. Kila siku itabaki kuwa historia na kuwa na jambo litakalo sadia kutengeneza maisha yetu ya baadaye. Kila siku Mungu anayokupa kuamka asubuhi, kwenda kufanya shughuli zako na kurudi nyumbani kwenye familia yako ni siku ya kumshukuru Mungu. Kuna wengi walilala usiku lakini hawakuamka, lakini wewe umeamka. Kuna wengi waliamka asubuhi na kwenda kwenye shughuli zao lakini hawakurudi jioni lakini wewe umepata neema ya kurudi nyumbani. Mshukuru Mungu, mtukuze kwa kukupa nafasi ya kuona siku ya leo. Kumbuka amekuacha hadi leo maana ana kusudi na maisha yako. Mshukuru Mungu kwa yote katika maisha yako na endelea kumtumaini bila kukata tamaa.Ukiona bado unaishi basi ujue ni neema ya Mungu pakee na sio uweza wako. Basi ndugu zanguni tuzidi kumuomba Mungu Ili mapenzi yake yatimizwe.

SALA: Mungu wangu, nakushukuru kwa siku ya leo. Nitie nguvu nifanye yote nayotakiwa kufanya siku hii ya leo. Kwa Jina la Yesu, Amina.
(c)IYK_Neno